Saturday, March 24, 2012
ABOUT BARAKA
Tunao vijana au hatuna?
Anaingia darasani,ananikuta nina gazeti makini kwa watu makini “Gazeti la Raia Mwema”.Anaomba gazeti na mimi ninampatia.Kuna mtu ana swali lolote?baada ya sekunde kadhaa kupita,nina muuliza swali linalohusiana na maisha ya vijana na mustakabali mzima wa taifa letu.Ni kawaida yangu kumuuliza maswali mwalimu wa tutorial wa somo la development studies.Na wanafunzi wenzangu wananijua kwa tabia yangu ya udadisi na ujengaji wa hoja kwenye masuala ya msingi.Kabla ya kunijibu,ananiuliza;kwani kijana ni nani?
Mimi:Kijana ni mtu aliye na umri wa miaka 15 mpaka 35,kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007.
Wanafunzi wengine wanatoa maana ya kuwa kijana,kila mmoja kwa mtazamo wake na jinsi anavyofahamu.
Mwalimu:Na mimi ni kijana?
Wanafunzi:Mhhh…(wanaguna kidogo,kisha wanajibu huku wakitabasamu)..unatoka kwenye ujana na unaingia utu uzima.
Darasa zima kwa pamoja lina cheka.
Mwalimu:Mimi bado naona sija litumikia taifa kisawasa na taifa bado linaniitaji(anaendelea)katika mataifa ya wenzetu,ukionyeshwa CV ya kijana mwenye miaka 21,unaweza kusema-huyu anaelekea kustaafu,amefanya mambo yote haya.
Darasa linaangua kicheko,kisha linarudi katika hali yautulivu na kuendelea kupata busara za mwalimu.
Mwalimu:kuna vijana wanaoweza kuhakikisha na kufwatilia mchakato mzima wa uwepo wa baraza la taifa la vijana,maana wale wanaoona kuna umuhimu wa kuwa na baraza la vijana,ndiyo wanatoka katika ujana(anaanza kujibu,na kueleza kiundani maisha ya vijana wa Tanzania).
Mwalimu:Hatuna vijana katika nchi yetu.
Mimi:(katika hali ya kushangaa na kufikiri kwa haraka),mwalimu tunao vijana,wapo!
Mwalimu:hatuna vijana kwa maana halisi ya ujana.Katika taifa letu kuwa kijana ni,kuwa na simu ya ghararma na ya kifahari na kuibonyezabonyeza kila wakati,kujiunga na program za simu zinazokuwezesha kutuma message nyingi(exteme),kuweka earphone masikioni.
Sasa nina muuelewa vizuri mwalimu,ana maanisha taifa letu lina vijana wengi sana,walio katika umri ambao ni wa ujana(ujana kwa kigezo cha umri),ila limekosa vijana wengi,wenye fikra makini,wanaofikiri kwa undani na kutenda matendo yanayoifanya Tanzania,pawe mahali salama na penye maendeleo ya kweli yanayomgusa kila mtanzania kwa nafasi yake aliyonayo.
Mwalimu,anaendelea. “vijana wengi wanaishi maisha yasiyoeleweka na hawaelewi wanataka kufanya nini maishani mwao.Utawakuta ikikaribia weekend,wanaulizana,weekend hii kiwanja gani.ikifika jumatatu,utawaona kwenye magazeti ya udaku wakipekua,ili wajue nani alikuwa na nani weekend,nani anaskendo gani,nani alifunika weekend”.
Sasa ukishafika mahali ukiwa na vijana wengi wa namna hiyo kwenye taifa,ni hatari.Unaweza ukapata picha na ukajua hali ya vijana walio wengi wa kitanzania.
Vijana wengi wemejikita kwenye masuala ya starehe na anasa zaidi kuliko masuala ya msingi naya maendeleo.Tatizo lililopo leo hii,vitu vya msingi na vya maana,tumevidharau na kuvifanya vionekane havina maana,tumekumbatia vitu vya kipuuzi na kipumbavu na tumevipa kapao mbele katika maisha yetu kuliko vyenye maana.Tukiendelea na hali hii,hatutafika na hata tukifika,tutakuwa tumefika mahali ambapo hatukustahili kufika hapo pabaya.
Kwa muda mrefu nimeishi mkoa wa Mbeya.Wilaya ya Mbeya mjini,nilifahamiana na vijana wengi.Na hivyo nina diriki kusema kwa asilimia kubwa(70 au 80)nina wafahamu vijana wa Mbeya.
Mwaka 2009,nilijiunga na shule ya wavulana songea(songea boys’)kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita,katika mchepuo wa P.C.B(physics,chemistry and biology),mwaka 2011 nilihitimu.Huko nako songea nilikutana na kufahamiana na vijana.
Kwa sasa,ninaishi,Dar Es Salaam.Hapa napo ninafahamiana na kukutana na vijana.
Nimekuwa nikifuatilia na kujihusisha na harakati za vijana,katika kuishi kwangu takribani mikoa mitatu na kujihusisha na harakati za vijana.Nimegundua kitu kimoja, ‘’ vijana wengi wanaelekeana jinsi wanavyo yaendesha maisha yao,na kuna vijana wachache sana hawaelekeani na hawaendani na hao walio vijana wengi’’.Ukimchukua kijana wa Mbeya,kisha ukawaleta vijana wa mikoa ya Dar,Mwanza,Arusha,Mara,Bukoba,Iringa na Morogoro,utagundua kuna values wana share(shared common values of Tanzania youth).Na hiki ndicho kinachowatofautisha na vijana wa Botswana,Zambia,Afrika kusini na mataifa mengine.
Kunaa baadhi ya jamii duniani huwa thamini vijana wao.na jamii hizo huamini vijana ndiyo injini ya maendeleo ya sasa naya baadaye, ,hivyobasi kuna kila haja ya kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi bora,wazazi na walezi bora,wafanya kazi wanaojituma katika kazi zao.jamii yeyote inayowathamini vijana,huwajengea vijana uwezo katika mambo mbalimbali,huwapa elimu bora inayofanya wastaarabike,wawe wadadisi,wabunifu.lakini kuna baadhi ya jamii,huwaona na kuwachukulia vijana,kama watu wasio staarabika,watu walio na ubaya na vurugu za kila aina,waliokosa heshima,wenye matendo maovu.Kuna sababu nyingi zinazosababisha mpaka jamii iwachukulie vijana kwa mtazamo huo,lakini moja ya sababu hizo ni maisha ya vijana jinsi wanavyokuwa wanaishi katika jamii hiyo, “huwezi ukaonekana kijana mwenye vurugu,kama vurugu siyo maisha yako”.Kijana atachukuliwa amestaarabika,iwapo tu ustaarabu ni maisha yake.
Tunao vijana waliostaarabika na wenye uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo katika taifa.Vijana wa namna hii,tunawaitaji sana,ingawa ni wachache sana.Leo hii vijana wengi wanaishi maisha yaliyokosa dira.Kijana anaweza akawa amesoma na bado maisha yake ya kakosa dira.Mara nyingi vijana waliokosa dira,hufanya lolote wanalojisikia,pasipo ata kutafakari kwa ndani,matokeo yanayoweza kutokea hapo baadaye,vijana wa namna hii wala hawana habari na kufanya tathmini ya maisha yao,kujielimisha kwao siyo suala la msingi.Tumefika mahali tumesaha ya kwamba kila kijana ana wajibu wa kujielimisha yeye mwenyew binafsi.Kijana anaweza akajielimisha kwa kusoma vitabu(achilia mbali vya darasani)kwa bahati mbaya tumehalalisha ya kwamba kusoma vitabu siyo utamaduni wetu na wala hautuhusu,kwa kushiriki mijadala,makongamano,midahalo inayochambua masuala ya msingi,kwa kukaa na wenye busara na kujifunza kutoka kwao,kwa kufuatilia habari za muhimu katika vyombo vya habari,kwa kutembelea mitandao ya maana na inayomjengea kijana uwezo wa kufikiri..bahati mbaya leo hii vijana walio wengi wanaishi maisha yasiyoakisi maana halisi ya ujana,wanaamini katika mambo ya kipuuzi yasiyotakiwa kuaminika,waliojawa na hofu na wamekosa udhubutu kwenye masuala yanayowaletea maendeleo yao ila wana udhubutu kwenye mambo ambayo siyo ya msingi.Mijadala yao mingi imejikita kuwazungumzia watu,hawataki kuongelea uhalisia wa maisha.
Wewe mazungumzo yako,yana husu nini?
Unafikiri nini?
Matendo yako?
Jitathmini,jitafakari,kisha amua unataka mfumo gani wa maisha,ukishaamua mfumo unaotaka kuufuata hakikisha unakuwa na msimamo madhubuti.
Huu ni wakati wa kubadili fikra zetu,na kusimamia usahihi,haki na wajibu.Tunuie toka ndani yetu,kuleta mabadiliko katika taifa hili.Wakati wa kuzubaa umeisha,wakati wa kulalamika umeisha,hatuna tena muda wa kuogopa.Kama kila kijana atatambua na kutimiza wajibu wake,tuwe na uhakika tutapata jamii ya vijana wanaowajibika,wanaowajibika kwa kumfuata Mungu,wanaowajibika katika familia zao,wanaowajibika katika masuala ya maendeleo ya taifa hili.UJANA NI FIKRA MAKINI,AMUA KUWA NA FIKRA MAKINI UWE KIJANA.
Na; Baraka Daniel Kiranga.
+255762362413.